Katika taifa lolote duniani, shughuli za binadamu ndio huchangia kwa kiasi kikubwa katika pato/uchumi wa taifa husika. Shughuli hizo hizo kwa jinsi moja au nyingine huchangia kwa kiasi kikubwa aidha kukuza uchumi wa nchi husika, ama kuchafua mazingira na pengine kuua hata mazalia mbalimbali ya viumbe hai na kushusha uchumi. Hivyo, sera za nchi husika ndio huamua aidha nchi ifaidike na mazingira yake au iendelee kudumaa kiuchumi, ilihali ina kila rasilimali ambazo zinaweza kuikwamua kiuchumi.
Tanzania ni nchi yenye mazingira mazuri na ya kuvutia, mbuga nzuri zenye wanyama na ndege wa kila aina- ambazo kwa muda mrefu zimekuwa kivutio kikuu kwa watalii. Ukichunguza kwa undani utagundua kuwa, mazingira/maliasili ya nchi yetu ndio inatupatia heshima kubwa watanzania-kuanzaia mlima Kilimanjaro, Mbuga mbali mbali zijulikanazo duniani kote, Maziwa na mito mikubwa mpaka katika majina ya viburudisho kama Kilimanjaro, Ndovu na Serengeti- yote katika kutangaza mazingira ya mtanzania.
"Kwa ujumla, mazingira ni muhumu sana kwani yanaipatia nchi mahitaji yote ya msingi kwa ajili ya kufanikisha masuala ya jamii na uchumi. Mazingira ndiyo makazi ya viumbe vyote – mimea na wanyama ambao ndiyo urithi usiokuwa na badala yake. Mazingira ni chombo cha kuweka yale yasiyofaa. Mazingira ni msingi ambao ndiyo itakuwa jawabu la kupunguza unyonge wa umaskini." Pia, sekta ya maliasili, mazingira na utalii inachangia zaidi ya 14% ya bajeti ya Tanzania.